Hapiness Magesse: Nilifanyiwa upasuaji mara 12 kunusuru kizazi changu bila mafanikio, mwisho wa siku kizazi kilitolewa

Februari  ya  kila  mwaka  huenda  ikawa  ni  kumbukumbu  mbaya  kwa  mwanamitindo  na  Miss Tanzania  2001, Hapiness Millen  Magese  ambaye  mwezi  huo  ndipo  alipogundulika  kuwa  hataweza  kupata  mtoto  katika  maisha  yake  yote.....


Hali  hiyo  ndio  imemlazimu  mwanamitindo  huyo  kuanzisha  taasisi  ya  kuwasaidia  wanawake  wengine  hapa  nchini  ili  waepuke kile  ambacho  kimemkuta  yeye  baada  ya  kuondolewa  uzazi  kwa  ugonjwa  ambao  hapendi  kusikia  unamtokea  mwanamke  mwingine.....

"Nikiwa  sekondari  nilikuwa  napatwa  na  ugonjwa  ambao  kwa  wakati  huo  niliona  ni  wa  kawaida.Nilikuwa  napata  maumivu  makali  wakati  wa  hedhi  yaliyonisababishia  kutapika  na  wakati  mwingine  kupoteza  fahamu," anasema.

"Kila  nilipoingia  kwenye  hedhi  nililazimika  kulazwa  kwa  siku  sita  hadi  kumi  hospitalini,kutokana  na  maumivu  hayo  kuna  wakati  wanafunzi  wenzangu  waliwahi  kunihoji  ni  kwa  nini  mimi  kila  mwezi  lazima  niugue,"  anasimulia

Anasema  ilifika  wakati  wakawa  wanamhesabia  tarehe  kutoka  siku  anayotoka  hospitali  hadi  mwezi  mwingine  atakapolazwa  tena

"Niliteseka  sana, nakumbuka  kuna  siku  nilizidiwa  wakati  mama  yangu  hayupo.Baba  akachukua  jukumu  la  kunibeba  na  kunipeleka  hospitali," anasema.

"Nilipokuwa  kwenye  maumivu  makali  aliniambia  nijikaze  kama  mwanamke,  hivyo  nikawa  namficha  baba  maradhi  yangu, ingawa  ilikuwa  kila  mwezi  kama  siyo  kunipeleka  hospitali  yeye  basi  lazima aje  kunitazama  hospitali."

Anasema  hata  baada  ya  kujiingiza  kwenye  masuala  ya  urembo, bado  hali  ya  maumivu  wakati  wa  hedhi  iliendelea  na  siku  alipoamua  kujiingiza  kwenye  uanamitindo  kuna  watu  walimuuliza  atamudu  kweli  kufanya  mitindo  na  hali  aliyonayo?

"Nikiwa  hapa  nyumbani  sikujua  nasumbuliwa  na  nini. Siku  moja  nikaamua  kwenda  kupima  wakati  huo  nikiwa  Afrika  Kusini, nikagundulika  kuwa  na  ugonjwa  wa  Endometriosis   na  tiba  pekee  ikawa  kufanyiwa  upasuaji,"  anasema  Magese.

Anasema  alifanyiwa  upasuaji  mara  ya  kwanza  na  kuonyesha  yai  lake  moja  ni  bovu  hivyo  kutakiwa  litolewe  ingawa  alikuwa  na  uwezo  wa  kubeba  mimba.

"Nilifanyiwa  upasuaji  mara  ya  pili,kila  siku  nikalazimika  kuwa  nafanyiwa  uchunguzi  ili  kubaini  maendeleo  ya  hali  yangu, lakini  cha  kushangaza  hali  ilizidi  kuwa  mbaya.Kuna  wakati  nilijiuliza  kwa  nini  mimi?"  anasema  Magese.

Anasema  katika  kipindi  hicho  alikuwa  anachoma  sindano  kila  asubuhi  kwa  siku  63  ili  kunusuru  kizazi  chake  bila  mafanikio, aliendelea  kufanyiwa  upasuaji  mara  12  zaidi.

Endometriosis  ni  nini?  Dalili  zake  ni  zipi?
Daktari  bingwa  wa  magonjwa  ya  akina mama  na  uzazi  wa  Hospitali  ya  Taifa  Muhimbili, Dr. Fadhlun  Almy  anasema  bado  hajapata  jina  la  Kiswahili  la  ugonjwa  wa  Endometriosis, lakini  unasababishwa  na  seli  za  tumbo  la  uzazi  kuwa  nje   ya  kizazi.

"Dalili  za  ugonjwa  huu  ni  maumivu  makali  wakati  wa  hedhi  na  maumivu  hayo  yanasababisha  makovu  ndani  ya  ukuta  wa  tumbo.Makovu  hayo  yakizidi  yanasababisha  mirija  ya  uzazi  kuungana  na  Ovari," anasema

0 Response to "Hapiness Magesse: Nilifanyiwa upasuaji mara 12 kunusuru kizazi changu bila mafanikio, mwisho wa siku kizazi kilitolewa"

Post a Comment