MSANII maarufu wa vichekesho nchini Musa Yusuf 'Kitale', ambaye kwa sasa amekuwa maarufu kwa jina la Mkude Simba, juzi alipagawisha katika tamasha la burudani la utambulisho wa kituo kipya cha Redio cha Efm 93.7 kwenye viwanja vya TP Manzese, Dar es Salaam.
Tamasha hilo lilikuwa ni la pili, ikiwa ni baada ya kufanyika katika Wilaya ya Temeke wiki mbili zilizopita na kushuhudia umati wa wakazi wa wilaya hiyo na maeneo ya jirani wakifurika kwa wingi katika viwanja vya Mwembe Yanga.
Katika tamasha la juzi, mbali ya Mkude Simba, wasanii wengine waliopagawisha ni mkali wa Hip Hop nchini, Fareed Kubanda ‘Fid Q’, Haruna Kahena ‘Inspector Haroun’, Pacha wa Ngwea, vikundi mbalimbali vya mchiriku na wasanii wengine wengi kutoka Kinondoni na maeneo mengineyo jijini Dar es Salaam.
Tamasha hilo lililoanza takribani saa nne asubuhi na kumalizika saa 10:15, lilikuwa la aina yake kutokana na mahudhurio ya watu wa rika mbalimbali, huku Mkude Simba akikonga nyoyo za umati huo kutokana na mtindo wake wa uchekeshaji ulioasisiwa na Efm.
Kwa upande wake, Inspector Haroun alikumbushia enzi zake kwa kuimba nyimbo zake za zamani na mpya kama vile Asali wa Moyo, Mtoto wa Geti Kali na nyinginezo, wakati Fid Q alifanya kweli na ngoma zake kama Siri ya Mchezo, Propaganda, Chagua Moja na nyinginezo.
Mbali ya wasanii hao, Pacha wa Ngwea pia alitoa burudani ya nguvu kama ilivyokuwa kwa vikundi mbalimbali vya Mchiriku na kuifanya siku hiyo kuwa ya kipekee kwa wakazi wa maeneo hayo na wapitanjia kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa shoo hiyo, Msemaji wa Efm, Samira Kiango, alisema kuwa wameona wafanye hivyo kama sehemu ya kujitambulisha kwa wakazi wa Dar es Salaam, wakiwa wameanza kufanya hivyo katika Wilaya ya Temeke na kwamba wiki mbili zijazo watahamia Ilala kwenye viwanja vya Jangwani.
“Ikumbukwe kabla ya tamasha hili, tulitoa msaada wa vitu mbalimbali vya kufanyia usafi katika Hospitali ya Palestina iliyopo Sinza, ikiwa ni sehemu ya kuonyesha jinsi ambavyo tunaguswa na masuala ya kijamii. Tamasha lijalo litafanyika kwenye viwanja vya Jangwani, Ilala ambapo litakuwa la aina yake kwa kujumuisha wasanii wakubwa na chipukizi,” alisema.
Kituo cha Redio cha Efm, kimeanzishwa miezi mitatu iliyopita ambapo tayari kimejizolea umaarufu miongoni mwa wakazi wa Dar es Salaam, kikiwa kimepania kutoa burudani ya nguvu kwa wakazi wa jiji hilo, chini ya kauli mbiu yao, ‘Muziki Unaongea’.
0 Response to "Mkude Simba, Fid Q, Pacha wa Ngwea usipime Tamasha la Efm."
Post a Comment