Februari ya kila mwaka huenda ikawa ni kumbukumbu mbaya kwa mwanamitindo na Miss Tanzania 2001, Hapiness Millen Magese ambaye mwezi huo ndipo alipogundulika kuwa hataweza kupata mtoto katika maisha yake yote.....
Hali hiyo ndio imemlazimu mwanamitindo huyo kuanzisha taasisi ya kuwasaidia wanawake wengine hapa nchini ili waepuke kile ambacho kimemkuta yeye baada ya kuondolewa uzazi kwa ugonjwa ambao hapendi kusikia unamtokea mwanamke mwingine.....
"Nikiwa sekondari nilikuwa napatwa na ugonjwa ambao kwa wakati huo niliona ni wa kawaida.Nilikuwa napata maumivu makali wakati wa hedhi yaliyonisababishia kutapika na wakati mwingine kupoteza fahamu," anasema.
"Kila nilipoingia kwenye hedhi nililazimika kulazwa kwa siku sita hadi kumi hospitalini,kutokana na maumivu hayo kuna wakati wanafunzi wenzangu waliwahi kunihoji ni kwa nini mimi kila mwezi lazima niugue," anasimulia
Anasema ilifika wakati wakawa wanamhesabia tarehe kutoka siku anayotoka hospitali hadi mwezi mwingine atakapolazwa tena
"Niliteseka sana, nakumbuka kuna siku nilizidiwa wakati mama yangu hayupo.Baba akachukua jukumu la kunibeba na kunipeleka hospitali," anasema.
"Nilipokuwa kwenye maumivu makali aliniambia nijikaze kama mwanamke, hivyo nikawa namficha baba maradhi yangu, ingawa ilikuwa kila mwezi kama siyo kunipeleka hospitali yeye basi lazima aje kunitazama hospitali."
Anasema hata baada ya kujiingiza kwenye masuala ya urembo, bado hali ya maumivu wakati wa hedhi iliendelea na siku alipoamua kujiingiza kwenye uanamitindo kuna watu walimuuliza atamudu kweli kufanya mitindo na hali aliyonayo?
"Nikiwa hapa nyumbani sikujua nasumbuliwa na nini. Siku moja nikaamua kwenda kupima wakati huo nikiwa Afrika Kusini, nikagundulika kuwa na ugonjwa wa Endometriosis na tiba pekee ikawa kufanyiwa upasuaji," anasema Magese.
Anasema alifanyiwa upasuaji mara ya kwanza na kuonyesha yai lake moja ni bovu hivyo kutakiwa litolewe ingawa alikuwa na uwezo wa kubeba mimba.
"Nilifanyiwa upasuaji mara ya pili,kila siku nikalazimika kuwa nafanyiwa uchunguzi ili kubaini maendeleo ya hali yangu, lakini cha kushangaza hali ilizidi kuwa mbaya.Kuna wakati nilijiuliza kwa nini mimi?" anasema Magese.
Anasema katika kipindi hicho alikuwa anachoma sindano kila asubuhi kwa siku 63 ili kunusuru kizazi chake bila mafanikio, aliendelea kufanyiwa upasuaji mara 12 zaidi.
Endometriosis ni nini? Dalili zake ni zipi?
Daktari bingwa wa magonjwa ya akina mama na uzazi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dr. Fadhlun Almy anasema bado hajapata jina la Kiswahili la ugonjwa wa Endometriosis, lakini unasababishwa na seli za tumbo la uzazi kuwa nje ya kizazi.
"Dalili za ugonjwa huu ni maumivu makali wakati wa hedhi na maumivu hayo yanasababisha makovu ndani ya ukuta wa tumbo.Makovu hayo yakizidi yanasababisha mirija ya uzazi kuungana na Ovari," anasema
0 Response to "Hapiness Magesse: Nilifanyiwa upasuaji mara 12 kunusuru kizazi changu bila mafanikio, mwisho wa siku kizazi kilitolewa"
Post a Comment