WAGANGA WANAO TIBU KWA KUTUMIA NGONO NA NGUO ZA NDANI WAKAMTWA DAR ES SALAAM

POLISI Mkoa wa Temeke, imewakamata vijana wawili wanaodaiwa kujifanya waganga wanaotoa tiba kwa wanawake, ambayo masharti yake ni kushiriki nao ngono bila kinga na kuacha nguo za ndani, ili zifanyiwe dawa zaidi. 

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Englibert Kiondo, alidai vijana hao Juma Hemedi (32) na Abrahman Mulsin, wote wakazi wa Tandika, baada ya kushiriki ngono na wagonjwa wao huwaambia waache nguo za ndani. Kamanda Kiondo alidai baada ya kupata malalamiko, Jeshi la Polisi lianzisha msako na kuwapekua waganga hao, ambapo walikutwa na nguo za ndani za kike 22, ambazo alisema zitakuwa ushahidi wa kuingiliwa kimwili kwa wanawake hao. Vitu vingine wanavyodaiwa kukutwa navyo ni pembe, tunguli, makopo ya dawa na vibuyu. “Sheria iko wazi, inasema mganga anapofanya ngono kama uganga anakuwa amebaka, na hii ni kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni ya Adhabu 130 sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002,” alisema Kamanda Kiondo.

Kwa mujibu wa madai ya Kamanda Kiondo, vijana hao wamekuwa wakijifanya waganga wa tiba asili, husambaza vipeperushi sehemu mbalimbali za jiji kutafuta wateja. Mbali na tiba hiyo ya kupata watoto, inayotolewa kwa kushiriki ngono na mganga, Kamanda Kiondo alidai watuhumiwa hao wamekuwa wakidai kutibu magonjwa mengine kama kisukari, vidonda vya tumbo, nguvu za kiume, kukuza maumbile, kupata kazi, kufaulu mtihani, mvuto wa biashara, kumilikishwa jini na kupewa pete ya bahati. 

Katika tukio lingine, Polisi inamshikilia kijana mwingine mkazi wa Tandika Devis Corner, Maalim Kimti Rita au kwa jina lingine, Joseph Rita anayedaiwa kutapeli Sh milioni 11 akijidai kumfanyia dua mfanyabiashara aweze kukuza biashara yake. Alidai kuna mfanyabiashara mwanamke ambaye alitoa Sh milioni 11 kwa Maalim Rita, akidanganywa kuwa atafanyiwa uganga ili afanikiwe katika biashara yake, lakini alipoona hakuna alichopata, akaamua kutoa taarifa Polisi. 

Kamanda Kiondo alisema jamii inapaswa kuelimishwa kuachana na mambo hayo, kwa sababu tiba yake haipo kwa waganga wa jadi na kwamba hakuna uhusiano kati ya kufaulu na kwenda kwa waganga isipokuwa bidii ya kazi. “Watu wengi wamelalamikia matukio ya namna hiyo, sasa tumeamua kuweka wazi kwa umma kwa kuwa watu wanateketea kwa kukosa elimu… watu wanauza nyumba magari na mali zao, kwa ajili ya kupata fedha za kupeleka kwa waganga wakiamini kuna tiba, huu ni utapeli vijana kama hawa hawawezi kukupa utajiri wala mtoto,” alisema Kamanda Kiondo. Alisema waganga hao wamepata vyeti vya kufanyia kazi hiyo ya uganga wa jadi, lakini wanachofanya ni kinyume na kazi hiyo ambapo aliahidi vyeti vyao kuchunguzwa, kuona wamevipataje na kuwasiliana na Wizara ya Maliasili na Utalii, ili watambue pembe wanazotumia ni za mnyama gani.

0 Response to "WAGANGA WANAO TIBU KWA KUTUMIA NGONO NA NGUO ZA NDANI WAKAMTWA DAR ES SALAAM"

Post a Comment