Undani wa Sakata la Mnenguaji wa Kundi la Kanga Moko aliyepigwa Risasi na Askari Polisi

Mnenguaji  wa Kundi la Kanga Moko, Zawia Hamis  ambaye usiku wa Jumatano iliyopita alipigwa risasi mbili mwilini  na mtu aliyedaiwa ni askari polisi, ameweka undani wa sakata hilo.

Akizungumza na Risasi Jumamosi  juzi nyumbani kwake Mwananyamala jijini Dar, majeruhi huyo alisema tukio hilo lilijiri maeneo ya Mwananyamala- Kisiwani karibu na Ofisi za Chama cha Wananchi (Cuf) na kuongeza kuwa, kisa ni kubishana na askari huyo aliyetaka kuzimwa kwa matarumbeta kutoka kwenye kikundi chao kilichokuwa kikipita eneo hilo.
 
“Sisi tulikuwa tukipita na matarumbeta, askari wakatusimamisha na kutuamuru tuyazime kisha kutaka kutukamata watupeleke kituoni eti serikali imekataza.
 
“Tuliwaambia mbona ni mapema sana kwani ilikuwa saa kumi alasiri na Kova alisema ngoma za Kanga Moko, Kigodoro na nyingine zisipigwe usiku. Pia tuliwaambia tulichokuwa tukikifanya si ngoma hasa, ni matarumbeta tunapita kuwaalika watu kuwa leo kuna shughuli sehemu.

“Baada ya majibu hayo ndipo askari mmoja hakutaka hata kuendelea na mazungumzo, alitoa bastola kiunoni na kunipiga risasi mbili, moja kiunoni, nyingine kwenye mbavu halafu akapiga tena hovyo hewani risasi zilizobaki. Kwa kweli nimeumia sana,” alisema Zawia.
Mnenguaji huyo alisema kutokana na hali yake kuwa mbaya alipelekwa Kituo cha Polisi cha Mwinjuma na kupewa Polisi Fomu No. 3 (PF3) kisha kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kinondoni, Mwananyamala kwa ajili ya matibabu ambapo  kwa mujibu wake alitolewa risasi mbili. 

Baada ya kuzungumza na majeruhi huyo, waandishi wetu walikwenda kwenye Kituo cha Polisi Mwinjuma ambako ndiko alikoripoti PF3.
 
Askari mmoja wa kituo hicho (jina lipo) alisema hawezi kusema lolote kuhusu tukio huku akiweka wazi kwamba, afande aliyempiga risasi mnenguaji huyo anajulikana hivyo mlalamikaji anaweza kwenda mbele ya sheria.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Dar, Camillius Wambura hakupatikana kwa simu juzi kuzungumzia tukio hilo.

0 Response to "Undani wa Sakata la Mnenguaji wa Kundi la Kanga Moko aliyepigwa Risasi na Askari Polisi"

Post a Comment